Wakati Serikali ikibanwa na wabunge kwa kushindwa kutekeleza
Bajeti ya mwaka 2013/14 kutokana na kutegemea fedha za wahisani, Kamati ya
Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara imesema deni la taifa limeongezeka kwa
Sh8.2 trilioni kwa kipindi cha miezi saba tu.
Ilisema jana kuwa hadi Juni, mwaka jana deni hilo lilikuwa
Sh21.2 trilioni lakini hadi Januari mwaka huu, deni hilo lilipaa hadi Sh29.4
trilioni na fedha hizo zimekopwa kwa ajili ya kuendeshea warsha, semina,
safari, mafunzo na matengenezo ya magari.
Akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani, Waziri Kivuli wa
Fedha, James Mbatia alisema ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania
milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Sh600,000.
Kati ya Sh5.8trilioni za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka
2014/15, Sh4.3trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina
alisema Sh24.18trilioni ni deni la Serikali, Sh3.75trilioni ni deni la sekta
binafsi na Sh1.15trilioni ni deni la Benki Kuu Tanzania (BoT).
“Ongezeko hili la deni haliendi sambamba na kasi ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya uchumi. Hali hii inajenga
hofu kuwa huenda deni hili limekuwa ni uchochoro wa ubadhilifu wa fedha za
umma,” alisema Mpina.
Alisema licha ya Serikali mara kadhaa kueleza kuwa deni hilo ni
himilivu, kuna viashiria vinavyoonyesha kuelemewa kwa taifa na mzigo mkubwa wa
madeni.
“Mfano ni mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida
hivyo kuifanya Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari,
mafunzo na matengenezo ya magari,” alisema Mpina.
“Deni la Taifa sasa limefikia asilimia 47 ya Pato la Taifa na
kwa kipimo cha bei ya sasa deni la taifa limefikia asilimia 24, huku deni la
nje pekee likiwa ni asilimia 19” alisema Mpina na kuongeza:
“Licha ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)
kuahidi kwa muda mrefu kufanya ukaguzi maalumu wa deni la taifa, hadi sasa
taarifa yake haijawasilishwa. Ni lini taarifa hiyo itawasilishwa bungeni ili
kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa jambo hili?” alihoji.
Kamati hiyo pia iliilipua Serikali kwa kuuza mashine za
elekroniki (EFD), kati ya Sh600,000 hadi 700,000 kwa maelezo kuwa kiwango hicho
ni kikubwa kwa mzunguko wa biashara ya mtaji wa Sh14 milioni kwa sababu mtaji
wake hauzidi Sh5milioni.
Mpina alisema mashine hizo zinatakiwa kugawiwa bure kwa
wafanyabiashara wenye kipato chini ya Sh40milioni na kufafanua kuwa chombo
hicho chenye taarifa muhimu za mapato ya Serikali hakitakiwi kuuzwa na
kufanyiwa matengenezo na mtu binafsi.
Mpina alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na Mtandao wa Kimataifa
wa Global Financial Integrity (GFI), umebaini kuwa Tanzania inapoteza
Sh3trilioni kila mwaka kutokana na mzunguko wa fedha haramu.
“Kamati inataka taarifa ya mabilioni ya fedha zilizofichwa
katika Benki za Uswisi iwasilishwe mapema kabla Bunge halijaisha ili
kuwawezesha wabunge na wananchi kujua ukweli wa jambo hili,” alisema
No comments :
Post a Comment