News

Jaji Mexico akataa rufaa ya El Chapo


Jaji nchini Mexico ametupilia mbali rufaa iliyokuwa imewasilishwa na mlanguzi wa dawa za kulevya Joaquin "El Chapo" Guzman kupinga kupelekwa Marekania akajibu mashtaka


Wizara ya mambo ya nje ya Mexico iliidhinisha El Chapo akabidhiwe kwa maafisa wa Marekani lakini mawakili wa mlanguzi huo wamekuwa wakipinga uamuzi huo mahakamani.
Sasa, wamesema watakata rufaa katika mahakama ya juu.
Mkuu huyo wa genge la walanguzi wa mihadarati la Sinaloa alikamatwa mwezi Januari miezi sita baada yake kutoroka gerezani kwa kupitia njia ya chini ya ardhi iliyochimbwa hadi kwenye seli yake gerezani.
Alikuwa tayari ametoroka kutoka gereza la ulinzi mkali mara moja awali, na akakaa miaka 13 akitafutwa sana na maafisa wa usalama.
Kamishna mkuu wa usalama wa Mexico Renato Sales Heredia amesema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga kwamba Mexico inatarajia kumhamishia Marekani mshukiwa huyo "Januari au Februari".
Kupitia taarifa, afisi ya mwanasheria mkuu imesema jaji huyo "ameamua kukataa kinga" iliyokuwa imeombwa na Guzman.
Andres Granados, mmoja wa mawakili wa Guzman, amesema sasa watakata rufaa Mahakama ya Juu zaidi na ikibidi watawasilisha kesi hizo kwa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Nchi za Amerika.
"Hatujashindwa," ameambia shirika la habari la AFP.
Mexico ilikubali kumkabidhi Guzman kwa Marekani mwezi Mei baada ya kupata hakikisho kwamba hatakabiliwa na hukumu ya kifo.

Rais Magufuli atengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Pensheni wa LAPFi na kuvunja Bodi yote


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 21 Septemba, 2016 ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Pensheni wa LAPF Prof. Hasa Mlawa kuanzia leo.

Pamoja na kutengua uteuzi wa Prof. Hasa Mlawa, Rais Magufuli amevunja Bodi ya Udhamini ya Mfuko huo.

Uteuzi wa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Udhamini ya LAPF utafanywa baadaye.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

21 Septemba, 2016



CUF kugharamia matibabu ya Maalim Seif


Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF)  wamesema wapo tayari kugharamia matibabu ya Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif Sharif Hamad.

Tamko hilo limetolewa siku chache baada ya kuibuka taarifa kuwa  kiongozi huyo amesusa gharama za matibabu zinazotolewa na Serikali ingawa ni haki yake kwa mujibu wa sheria kama kiongozi mstaafu.

Akizungumza   kwa niaba ya wanachama wenzake kisiwani Unguja jana, mmoja wa wanachama wa CUF, Ali Abdallah Issa, alisema wanashangazwa na baadhi ya watu kumpiga na kumsema kiongozi huyo ambaye alidai ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha Wazanzibari.

“Maaalim ana haki zote za kuhudumiwa na Serikali na si vinginevyo. Lakini kwa manyanyaso na kusimangwa  kila kukicha sisi wanachama wa CUF tupo tayari kugharamia matibabu ya kiongozi wetu.

“Na hili si jambo geni, Maalim alikamatwa na kuwekwa kuzuizini.  Je, alipotoka  alikuwa akitibiwa na SMZ? Jibu ni hapana ni fedha zake mwenyewe binafsi pamoja na wana CUF ambao walikuwa mstari wa mbele kumhudumia kiongozi wetu nasi sasa tutafaya hivyo ikiwa SMZ imeshindwa,” alisema Ali.

Alisema kitendo cha Maalim Seif kusafiri nje ya nchi kwa matibabu bila ya huduma za Serikali hakileti picha nzuri.

Kuna hatari visiwa vya Zanzibar vikaingia katika mgogoro na kujengeka   chuki hasa kati ya CUF na CCM, alisema.

‘’Iwapo Maalim Seif amekwenda kwenye matibabu kwa gharama zake binafsi basi inasikitisha sana kuona ni jinsi gani Katiba inavyoanza kukiukwa na kwa kweli si jambo jema na halifai,” alisema.

Naye Is-hak Said Makame, alisema   Zanzibar imepita katika wakati mgumu hasa baada ya kutokea   migogoro ya siasa iliyotokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana  na ule wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

“Maalim hawezi kusemwa na hata kuonekana ni kiongozi anayetibiwa kwa fadhila kama alivyotaka Rais Magufuli alipokuja hapa Unguja kwenye mikutano yake. Sasa tunasema sisi CUF tutamlinda kiongozi wetu kwa hali na mali,”alisema Makame.

Alipotafutwa  Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Biman  kujua  Maalim Seif  amepata wapi fedha kwa ajili ya safari ya nje ya nchi kutibiwa.

Alisema  hajui ni wapi kiongozi huyo alipopata fedha za matibabu.

“Katibu Mkuu amekwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake lakini nasi hatujui ni wapi amepata fedha. Ila atakaporejea nchini itatolewa taarifa kwa kina kuhusu suala hili,” alisema Biman.

Maalim Seif yuko   India na anatarajiwa kujerea nchini siku chache zijazo.

Rais Magufuli Asema Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA itafunga ofisi katika nchi ya Rwanda......Pia Kasema Serikali Imetenga Trilioni 1 Kwa Ajili ya Ujenzi wa Reli Kwenda Rwanda


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam ni salama kwa wao kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Julai, 2016 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya habari wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.

Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuchukua hatua kadhaa za kuboresha bandari ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara wanaopitisha mizigo, Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi Mjini Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili.

Aidha, Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi wa Tanzania na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni moja katika bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni matarajio kuwa wadau wengine wa maendeleo watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku akidokeza kuwa China imeonesha nia ya kuunga mkono mradi huo.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amemhakikishia kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Majira ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji wake Rais Magufuli, amefungua rasmi maonesho ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam.

Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa nyingi za kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.

Nae Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani 30 zilizojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau zaidi ya 2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza biashara baina yake kwa kuwa hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi hizo ni cha chini mno.

Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame na mwenyeji wake Rais Magufuli wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na huduma katika viwanja vya Sabasaba na baadaye Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016
CUF yatangaza kutomtambua Dkt. Ali Mohamed Shein
Kufuatia ubakaji wa demokrasia kupitia kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio uliofanywa juzi tarehe 20 Machi, 2016, jana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alikamilisha kazi aliyoagizwa kwa kutangaza kile alichokiita matokeo ya uchaguzi wa Urais.
Chama Cha Wananchi (CUF) kilishaeleza msimamo wake kuhusu ubakaji huo wa demokrasia kupitia taarifa yake kiliotoa tarehe 18 Machi, 2016. Baada ya hatua ya jana tunaweka msimamo wetu kwamba:
1. Hatutambui hicho kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016 na kwa maana hiyo hatumtambui huyo aliyedaiwa kuwa mshindi na kwa msingi huo huo hatutoitambua wala kushirikiana na Serikali itakayoundwa kutokana na matokeo hayo batili ya uchaguzi batili.
2. Tunawapongeza kwa dhati Wazanzibari wote kwa ukomavu wao mkubwa wa kisiasa waliouonesha kwa kuitikia wito wa mpendwa wao Maalim Seif Sharif Hamad na chama chao cha CUF na kutoshiriki katika uchaguzi huo batili. Kwa ujasiri wao huo wameudhihirishia ulimwengu kwa njia za amani na za kistaarabu kwamba chaguo lao ni Maalim Seif Sharif Hamad. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameyathibitisha maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya kupitia uchaguzi huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
3. Tunavipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje na jumuiya ya kimataifa kwa kuonesha hali halisi ilivyokuwa na jinsi Wazanzibari walivyoikataa CCM, walivyowakataa watawala na walivyokataa kutumika kubaka demokrasia. Wazanzibari wameandika historia nyengine mbele ya macho ya ulimwengu. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameshinda.
4. Tunajua Wazanzibari wana hamu ya kujua hatua zinazofuata katika kusimamia maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015. Chama chao kinawatoa wasiwasi Wazanzibari kwamba hakijayumba na kinafuatilia haki yao hiyo kwa njia za amani na za kidemokrasia na kitakuwa kikiwaeleza kila kinachoendelea.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU – CUF
22 Machi 2016
Binti wa Miaka 17 Ajifungulia Mtoto Chooni Hospitali ya Amana Dar
Msichana wa umri wa miaka 17 ambaye alikuwa katika machungu ya uzazi, amejikuta akijifungulia mtoto chooni baada ya muuguzi mmoja wa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam kumtaka aende kuoga na kubadilisha nguo bila ya kujali hali yake.

Msichana huyo, Asha Sudi (17), mkazi wa Tabata Kisiwani, alikutwa na tukio hilo juzi wakati akisubiri kujifungua, na uongozi wa Amana umesema utalishughulikia suala hilo.

Asha alisema alifika hospitalini hapo saa 4:00 asubuhi akiwa anaumwa na uchungu na alipofika mapokezi alikalishwa kwenye benchi.

“Wakati nikiwa nimekaa kwenye benchi alikuja nesi akaniambia niende chooni nikaoge na kubadilisha nguo. Kwa sababu sikujua, nikaenda,”alisema Asha.

Alisema akiwa chooni anajiandaa kuoga, uchungu ulikata ghafla na baada ya dakika chache aliona kitu kinaning’inia sehemu za siri kisha kikadondoka chini.

Baada ya kuona hivyo, alianza kupiga kelele akiita “nesi, nesi” na ndipo alipopita wa kwanza ambaye hata hivyo hakumshughulikia na badala yake akaendelea na kazi zake, lakini baadaye akaenda daktari ambaye hakumtambua kwa jina, akamsaidia.

Nikiwa ninatapatapa sielewi alikuja daktari akamuokota mtoto ambaye alikuwa ameanguka chini karibu na tundu la choo,”alisema.

Baadhi ya wauguzi walitoa ushuhuda wa tukio hilo, wakiwamo daktari aliyemuokoa mama huyo na mwanaye chooni, lakini hawakutaka majina yao yatajwe

“Nilikuwa wodini. Wakati napita nikasikia mtu anapiga kelele chooni akiita ‘nesi, nesi, mwanangu jamani’. Nilishtuka, ikabidi niende kuona ndipo nikamkuta huyo binti akiwa amesima na kondo likiwa limening’inia na kitoto kichanga kimeanguka chini,” alisema.

Alieleza kuwa alikiokota kichanga hicho na mama yake kisha kuwapa huduma ya kumsafisha mtoto.

Muuguzi mwingine ambaye alikuwa zamu mchana, alisema alipopita kumuangalia mtoto huyo, alikuta akiwa na uvimbe kwenye paji la uso.

“Nikamuuliza mama wa mtoto ndipo akanisimulia. Kwanza nikashangaa huyu nesi ilikuwaje akamruhusu mama ambaye anataka kujifungua kwenda chooni?” alihoji.

Mkuu wa Idara ya Wazazi, Grace Massawe alisema wamelichukua suala hilo na kwamba watalishughulikia, lakini akawataka wazazi na ndugu wa mama huyo kuwa watulivu na kuwasamehe waliofanya tukio hilo.

“Mama tumekuelewa hili suala tutalishughulikia. Aliyefanya kosa hilo tutamuita. Najua alijisahau hasa ukizingatia bado ni mgeni, lakini tutalifanyia kazi,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto wa hospitali hiyo, Francis Kioweli alisema mtoto huyo hajapata athari ya kiafya na kwamba endapo kutatokea tatizo lolote, basi wazazi hao wasisite kwenda hospitali kwa uangalizi zaidi.
Breaking News: Tume ya Uchaguzi Zanzibar Yamtangaza Dr Shein Kuwa Rais wa Zanzibar

Baada ya uchaguzi wa marudio uliofanyika jana huko Zanzibar Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Yamtangaza Dr Shein Kuwa Rais wa Zanzibar.
DR SHEIN ASHINDA URAIS ZANZIBAR, KURA ALIZOPATA 299, 982 SAWA NA 91% YA KURA ZOTE ZILIZOPIGWA.
Video: Rais Magufuli ‘awakabidhi rungu” Wakuu wa Mikoa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Magufuli amewaapisha wakuu wapya mikoa leo na kuwataka wakawatumikie wananchi.
Rais Magufuli alisem kuwa; “Nimewateua ninyi (Wakuu wa Mikoa) muende mkawatumikie Wananchi na sio kwenda kufanya siasa.”
“Ilinichukua muda sana kuteua kwa sababu nilitaka kujihakikishia kuwa ninateua watu makini,” aliongeza.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mbele ya Waku wa Mikoa mara baada ya kuwaapisha leo Ikulu jijini Dar. Rais Dkt Magufuli amewapa siku 15 Wakuu wa Mikoa kuwaondoa watumishi hewa walio katika orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma katika Mikoa yao
Magufuli pia amewataka wakuu hao kuwa waende mikoani kutatua kero za elimu, ajira, ujambazi na nyingine kwa kushirikiana na viongoni wengine.
Lakini pia kiongozi huyo wa nchi alionya viongozi wanaonyanyasa wananchi bila sababu
Wakuu wa Mikoa wapya wa Tanzania Bara walioapishwa leo wakiwa katika picha ya pamoja Ikulu jijini Dar es Salaam
“Kuna viongozi huko wananyanyasa wananchi, unakuta katibu tarafa, mtendaji wa kata ananyanyasa tu wananchi bila sababu,” alionya.
“Ninyi mna mamlaka ya kumuweka mtu ndani hata masaa 48. Kawawekeni wengi ili kusudi wajue kwamba wananchi wanatakiwa kuheshimiwa.” alisema Rais.
Kauli Ya Abbas Kandoro Baada Ya Rais Magufuli Kutomchagua Kuwa Mkuu wa Mkoa
Jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe  Magufuli  alitoa orodha ya wakuu wapya wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Katika orodha hiyo Rais Magufuli , amewaacha wakuu kadhaa akiwamo aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Abbas Kandoro.

Kipindi cha Sun Rise cha Radio Times Fm, kimefanya mahojiano na Kandoro asubuhi ya leo, ambapo amekiri kuachwa kwake na kuongeza kuwa tayari amefikia kikomo cha uongozi kwa maana umri wake haumruhusu kuendelea kutumikia nyadhifa hiyo.

“Unajua kuna watu wakituona wanajua kwamba bado tupo kwenye ujana, Ndugu mtangazaji mimi nina miaka 66 sasa hivi, tayari umri umenitupa mkono katika nafasi hii.

“Haijanishtua kwa sababu wakati tunapewa hii mikataba tuliambiwa kabisa ukomo wa mkuu wa Wilaya ni miaka 60 na Ukuu wa Mkoa ni miaka 66, hivyo nmetimiza umri wangu kisheria na napenda nimshukuru Mh Rais kwa hili” Alisema Abbas Kandoro.

Mpaka kustaafu kwake, Kandoro amehodhi nafasi ya ukuu wa Mikoa katika zaidi ya Mikoa Sita Tanzania Bara ikiwemo Dar es salaam, Arusha, Singida na Mbeya.
CUF: Taarifa kwa vyombo vya habari
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, usalama wa raia wa Zanzibar na mali zao umekuwa katika hali tete.
Hali hii inatokana na kushuhudiwa kushamiri kwa matukio ya kuogopesha wananchi na kufurutu ada ukiukwaji wa HAKI ZA BINADAMU miongoni mwa wananchi kunakofanywa na vyombo vilivyopewa dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu raia wake na mali zao.
Katika siku za hivi kadribuni, hususan baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Sali Jecha, kutangaza kinyume na katiba ya nchi, kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 na matokeo yake, Zanzibar imeshuhudia uingizwaji na uingiaji mkubwa wa askari, vifaa na zana nzito za kivita katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Sambamba na hayo kumekuwepo kwa askari wengi wa JWTZ wanaorandaranda mitaani wakiwa na silaha nzito za kivita na operasheni isiyo rasmi ya kuwakamata na kuwabambikizia kesi wananchi wasio na hatia na hatimaye kuwaweka katika vituo mbali mbali vya polisi na kuwanyima dhamana hata kwa makosa ambayo kisheria yanapaswa kudhaminiwa.
Katika mwezi wa February 2016 huko Kengeja wafuasi wa CUF walikamatwa na polisi na kuwekwa ndani kwa tuhuma ya kuchoma tawi la CCM la eneo hilo. Polisi walichukuwa hatua hiyo mara tu tukio hilo liliporipotiwa kwao. Aidha katika mwezi huu wa Machi baadhi ya matawi ya CUF na Baraza za CUF zilichomwa moto na kuteketea tikitiki.
Taarifa ya uhalifu huu zilipripotiwa katika vituo vya polisi na RB kuandikwa, hata hivyo hadi hii leo hakuna yoyote aliyekamatwa kwa tuhuma ya uhalifu huo. Matukio ya uchomwaji moto na uharibifu wa mali za CUF umetokea mahala mwingi Unguja na Pemba kama vile Kisauni ambapo ofisi mpya ya CUF jimbo la Dimani zilizogharimu zaidi ya sh 90m zilichomwa moto tarehe 24/03/2015 na kuteketea. Kwa makusudi kabisa, hata baada ya polisi kupata taarifa hiyo na kulikagua eneo husika hakuna yeyote aliyetuhumiwa na kukamatwa.
Mtakumbuka kwamba tabia hii ya wananchi ambao kwa asilimia kubwa huwa ni CCM au vyombo vya serikali vilikuwa vikihujumu kwa makusudi mali ya CUF na hata mali ya serikali kama vile shule, zahanati, visima vya maji nk. Tukio la Shengajuu la 1996 ambapo watu waliofanya tukio la kcuhoma moto shule, kutia kinyesi visima walikamatwa wakiwa na petrol, bunduki, mapanga, madoo ya kinyesi vyote vikiwa usoni ya gari la idara ya usalama wa Taifa lenye namba za usajili ZNZ 1296).
Baada ya tukio hilo la kufedhehesha serikali na mapambamo yaliyofuata baina ya wafuasi wa CUF na wahalifu (usalama wa Taifa), serikali iliwaadhibu kwa kuwapiga, kuwaibia mali zao, kuwafanyia vitendo vya kinyama na kuwaweka ndani kwa zaidi ya miezi 9 wananchi wasio na hatia. Hivyo haya yanayoendelea hivi sasa huko Pemba si mambo mageni hasa katika kipindi hiki ambapo SMZ imechukia sana kwanini CUF wamegomea kushiriki uchaguzi batili wa madrudio wa 20/03/2016.
Sisi CUF tunaamini pasipo na shaka yeyote kwamba matukio ya kuchomwa moto kwa masikani na matawi ya CCM huko Pemba ama baadhi ya nyumba za watu binafsi na mali za serikali ni mwendelezo tu wa siasa chafu za chuki zinazoendelezwa na serikali dhidi ya wananchi wasio na hatia. CUF imesikitishwa sana na vitendo hivi vya kihuni na visivyoonyesha siasa za kistaarabu na inalaani vikali na kwa nguvu zote uhalifu huu ambao unarejesha nyuma ‘spirit’ ya kushindana bila kupigana.
Kwa upande mwengine, CUF imepokea taarifa kwamba zaidi ya wananchi 30 wengi wakiwa wafuasi, viongozi na wanachama wa CUF wamekamatwa na polisi na wameshikiliwa katika vituo mbali mbali vya polisi huko pemba. Utendaji huu wa Jeshi la polisi umeipelekea Zanzibar kugawika vipande vipande na kuwa chanzo cha siasa za chuki, uhasama na kusababisha nchi yetu kushindwa kutekeleza shughuli zake za kimaendeleo.
Kwa mfano amri ya Mkuu wa Mkoa kaskazini Pemba kupiga marufuku watu wasitembee baada ya saa mbili za usiku na kwamba atakayevunja amri hiyo atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la uzembe na uzururaji ni hatua nyengine ya SMZ ya kuwahalalilisha na kuwaweka wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba katika hali ngumu ya maisha. Amri hii inazuwia hata sala za Isha na Alfajiri jambo ambalo waumini wa Kiislamu hawatakubaliana nalo.
CUF inamtaka Mkuu wa Mkoa uliotajwa hapo juu awache ukereketwa na aendeshe mkoa kwa hekima, busara, na weledi. Kuongoza watu kwa amri za kidikteta kumepitwa na wakati. Asome alama za nyakati, aache kutoa amri zinazopingana na hata haki za binaadamu.
Chama Cha Wananchi CUF kinaamini kuwa kutokea kwa matukio haya ni mwendelezo wa njama za CCM zinazoratibiwa na kutekelezwa kimkakati kwa malengo mahususi ya kuamsha hamasa na kupandisha joto la jazba miongoni mwa wananchi ili kuhalalisha mpango maalum na kutoa fursa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutumika kutisha, kukamata, kupiga na kufungulia mashtaka wananchi wasio na hatia.
Kutokana na unyeti wake matukio ya uvunjifu wa amani na hatua za ukiukwaji wa HAKI ZA BINAADAMU, hayapaswi kupuuzwa kwani yanaweza kupelekea kufanikiwa kwa dhamira mbaya waliyonayo baadhi ya watu katika nchi yetu wasioitakia mema Zanzibar na kwa hivyo kuathiri umoja wa kimataifa uliopo uliopatikana kwa gharama kubwa ya jasho la viongozi wazalendo, Mheshimiwa Rais mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na uhai wa wananchi wanyonge. Kwa hivyo sisi katika CUF:
• Tunavinasihi vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu kukataa katakata kuingia katika mtego wa mipango miovu ya wanasiasa waliofilisika wenye lengo la kuleta taharuki miongoni mwa wananchi na kuamsha hamasa na kupandisha jazba na ghamidha zitakazopelekea kuchafuka kwa hali ya amani ya nchi yetu. CUF inatoa wito kwa kwa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama hapa nchini kusimamia amani na utulivu pasi na kuegemea upande wowote wa kisiasa.
Ni muhimu vyombo hivyo vikajipambanua na kujijengea heshima na kulinda imani ya wananchi waliyonayo kwao. Kinyume na haya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ, ambalo katika siku za hivi karibuni limeonekana kutumika vibaya, kufahamu kuwa mustakbali wa utu wa raia, mali zao na amani ya nchi yetu imo mikononi mwao na watakuwa wa mwanzo kuwajibika endapo jahazi la amani yetu litakwenda mrama.
• Tunaziomba Taasisi za kiraia za ndani kuacha woga na badala yake kupaza sauti zao masikioni mwa viongozi madhalimu kukemea unyanyasaji na ukandamizaji wa haki za binadamu. Aidha, CUF inaziomba jumuiya za kimataifa kuendelea kuitazama Zanzibar kwa umakini wa hali ya juu kufuatilia mwenendo na matukio na kuweka kumbukumbu kwa hatua za baadae kwa kila anaeonekana kushtadi kuonea wananchi wanyonge kutokana na nafasi yake katika utumishi wa umma.
• Tunatoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, John Magufuli, kuchukua dhamana ya uongozi kukataa kuhadaiwa na wasaidizi wake na kukomesha matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya amri yake na kudhibiti uhuni wa kisiasa wa baadhi ya watendaji wa vikosi vya Idara Maalum ya Zanzibar kama Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Kwa la zanzibar, Rais Magufuli hana pa kupenyea na kwamba atawajibika kutokana na mfumo wa Katiba, sheria na utaratibu wa kuongoza nchi tuliojiwekea.
• Tunatambua usumbufu, idhilali na mateso makubwa yanayowapata wananchi wa visiwa vyote vya Zanzibar kufuatia maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba 2015 ya kuikataa CCM na kuamua kufanya mabadiliko katika uongfozi wa nchi. CUF inawaomba wananchi wote kuendelea na kujipamba na mavazi ya subira na kuamini kuwa hizi ni hatua za mwisho za CCM kuelekea kufutika katika nyoyo za wazanzibari na kwamba wananchi wote wausiane katika kuvumilia na kukataa kuchokozeka kwa lengo la kutunza amani ya nchi yetu na kufikia malengo yetu ya muda mrefu ya kukamata hatamu za dola ya zanzibar bila kuathiri wanachi wetu.
• CUF inawahakikishia wananchi wote kuwa haitarudi nyuma katika mapambano ya kudai haki ya wananchi na kwamba maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba 2015 yatazingatiwa, kuheshimiwa na hatimaye haki kutamalaki katika visiwa vya zanzibar. Ni wajibu kwa Wazanzibari wote kutambua kuwa giza nene hufuatiwa na miale ya nuru inayotoa faraja kwa kila mwanandamu.
HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA
MAWASILIANO KWA UMMA
Paul Makonda atinga kortini, amkataa hakimu       
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda jana alitinga mahakamani na kumkataa hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi iliyofunguliwa dhidi yake na makada wawili wa zamani wa CCM wanaodai aliwakashifu.
Kesi dhidi ya Makonda, ambayo awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Hellen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilishafikia hatua ya utetezi na Makonda alitakiwa kuanza kujitetea jana, baada ya mahakama hiyo kumuona kuwa ana kesi ya kujibu.
Hata hivyo, jana Makonda ambaye ilifika mahakamani kwa mara ya kwanza tangu kesi hiyo ilipofunguliwa, alishikilia msimamo wa kutokuwa na imani na hakimu huyo na hivyo kuomba apangiwe hakimu mwingine.
Makonda alifikia msimamo huo kutokana na maneno aliyoelezwa na wakili wake, ambayo kwa mtazamo yalionyesha kuwa hakimu atakuwa anawapendelea wadai na hivyo asingemtendea haki.
Kutokana na madai ya Makonda, Hakimu Liwa amejitoa kwenye kesi hiyo na amepanga ianze kusikiliza upande wa mashtaka Machi 23.
Kesi dhidi ya Kubenea
Wakati Makonda akimkataa hakimu, mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea ameonekana ana kesi ya kujibu katika kesi inayomkabili ya tuhuma za kumtukana mkuu huyo wa wilaya. Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza kesi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Simba alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na mashahidi watatu, aridhika kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
Baada ya uamuzi huo wakili wa Kubenea, Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa mteja wake atajitetea kwa kiapo na kwamba watakuwa na mashahidi wanne na wanakusudia kuwaita wote mahakamani siku ya kujitetea.
Hakimu Simba alipanga mshtakiwa huyo aanze kujitetea Machi 7, mwaka huu.
Kubenea, ambaye alipandishwa kizimbani, mahakamani hapo Desemba 15, mwaka jana, anadaiwa kumtolea DC huyo lugha ya matusi Desemba 14 mwaka jana wakati wakiwa kiwanda cha Tooku Garments kilichoko Mabibo External, Kinondoni, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Anadaiwa kuwa siku hiyo alimuita Makonda kuwa ni “kibaka, mpumbavu na mjinga” na kwamba cheo chenyewe cha ukuu wa wilaya ni cha kupewa.
Wakati wa ushahidi wake, Makonda aliieleza mahakama kuwa alitumia nafasi yake ya ukuu wa wilaya kwenda kiwandani kwa lengo la kuzungumza na wafanyakazi waliokuwa wamegoma.
Mashahidi wengine wa upande wa mashtaka walikuwa ni maofisa wa polisi waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo.
Alisema alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi hao na kufunga kikao hicho, wakati anageuka alishangaa kumsikia mshtakiwa akimtukana.

Majambazi Dar es Salaam Yavamia Benki Ya Access....Yaua Mlinzi na Kupora Pesa, Polisi Wapambana Nayo na Kuyaua

 Majambazi  ambao  idadi  yao  haikufahamika  wakiwa  na  mabomu  na  bunduki  za  kisasa  jana  walivamia  Benki  ya  Access  tawi  la Mbagala  ambako  walipora  viroba vya   fedha, kuua  mlinzi  na  baadae wanne  kati  yao  waliuawa  na  jeshi  la  polisi.

Watu  walioshuhudia  tukio  hilo  walisema  baada  ya  majambazi  hao  kufika  katika  benki  hiyo  kwa  bodaboda  nne  majira  ya saa  nane  mchana,yalimuua  mlinzi  wa  benki  hiyo, kusha  kubomoa  kwa  risasi  mlango  wa  vioo  na  kuingia  ndani  na  kuzua taharuki  kubwa

Tairo  alisema  mbali  na  jambazi  huyo  kulipiga  risasi  gari  la polisi  pia  alilirushia  bomu  la  mkono,lakini  liliangukia  barabarani  bila  kuripuka.Polisi  walifanikiwa  kulilipua  bomu  hilo  baadae  likiwa  halijasababisha  madhara  kwa wananchi  waliofika  kushuhudia  tukio  hilo.

Mkazi  mwingine  wa  eneo  hilo,Rebecca  Maliva  alisema  majambazi  walioingia  ndani  ya  benki  hiyo  walioneka  wakitoka  na  viroba  vitatu vya  fedha  ambavyo  walivipakata kwenye  pikipiki  na  kuondoka  kwa  kasi  kuelekea  Mkuranga kupitia  barabara  ya  Kilwa.
Mashuhuda  hao  walisema, katika  tukio  hilo  lililodumu  kwa  karibu saa  moja,mmoja  wa  majambazi  hao  aliyekuwa  amevaa  kininja,alikuwa barabarani  akiamuru  magari  kupita  haraka  huku  akifyatua  risasi  hovyo.

Ilielezwa  kuwa, jambazi  huyo  aliyeonekana  kuwa  na  uzoefu  wa  matumizi  ya  bunduki  alikuwa  akifyatua  risasi  kwa  kutumia  mkono  mmoja  na  ndiye  aliyewajeruhi  baadhi  ya  wapita  njia.

Hivyo,wakati  uporaji  ukiendelea  na  jambazi  huyo  akiimarisha  ulinzi  barabarani  baadae  hakukuwa  na  magari  wala  pikipiki  zilizokuwa  zikipita.

Mfanyabiashara  wa  duka  la  vifaa  vya  ujenzi  jirani  na  benki  hiyo,Ramadhani Tairo  alisema  baada  ya  jambazi  huyo  kuliona  gari  la  polisi  likielekea  eneo  la  tukio,alifyatua  risasi  na kulipiga  kabla  halijafika.Gari  hilo  lilipoteza  mwelekeo  na  kutumbukia  mtaroni.
Rebecca  alisema  polisi  zaidi  walifika  kwenye  eneo  hilo  wengine  wakiwa  kwenye  pikipiki  na  kuanza  kuwafukuza  majambazi  hao  ambapo  walipofika  eneo  la  shule  ya  St. Marry's,walitupa  kiroba  kimoja  cha  fedha  ambacho  wananchi  waliokuwa    jirani  waligombania  na  kuchukua  fedha  zilizokuwemo  na   kisha  kila  mmoja  kukimbia  na  burungutu  la  noti.

Baada  ya  nusu  saa  wakati  umati  ukiwa  bado  upo  kwenye  benki  hiyo,magari  ya  polisi  yalipita  katika eneo  hilo  yakitokea  eneo  la  Mkuranga  yakiwa  yamebeba  miili  ya  majambazi  yaliyouawa.

Magari  hayo  yalikuwa  yakisindikizwa  na  vijana  wa  bodaboda  waliokuwa  wakishangilia  kazi  iliyofanywa  na  polisi.

Kamanda  wa  p[olisi  kanda  maalum ya  Dar es Salaam, Simon Sirro  alizungumzia  kwa  ufupi  tukio  hilo n kwamba  majambazi  manne  yaliuawa  na  kukamata  silaha  tatu,lakini  hakutaka  kuingia  kwa  ndani  akisema  atatoa  taarifa  zaidi  leo

Kikwete Kuwatumbua MAJIPU Wanachama Wasaliti wa CCM Waliokihujumu Chama Wakati wa Uchaguzi Mkuu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Jakaya Kikwete amesema kuwa chama chake kitawachambua na kuwaadhibu wote ambao walikisaliti katika Uchaguzi Mkuu uliopita, kuanzia ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa hadi Taifa.

Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo Jumatatu ya wiki hii mjini Kibaha alipohudhuria sherehe za uzinduzi wa ofisi mpya ya chama hicho mjini humo.

“Baada ya mchakato wa Dodoma wapo ambao walisusa kabisa na wakawa wanajificha. Unakuta hahudhurii mikutano yetu ya kampeni, lakini ya wenzetu upinzani unamkuta na akiulizwa anasema eti alialikwa,” alisema na kusisitiza kuwa wanachama kama hao ni wasaliti na uanachama wao una mashaka.

Kikwete alisema mchakato wa kuwaadhibu wanachama wasaliti utafanyika wakati wowote baada ya kuyapitia majina ya wote wanaotuhumiwa kukihujumu chama.

“Tayari tuna majina ya watu ambayo yanadhaniwa walikihujumu chama. Tutayapembua katika vikao mbalimbali halali kuanzia ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa na tutaamua kwa haki wakati wa kuwaadhibu,” alisema.

Aliwataka wanachama hao kufanya tathmini na kutambua waliokisaliti chama lakini alionya vikao vya kuwabaini vitende haki bila kumuonea mtu akisema yapo baadhi ya majina yanatajwa kuwa ni wasaliti kutokana na migogoro binafsi baina yao.


Meneja wa Shirika la Posta Tanzania Afikishwa Mahakamani Kwa Matumizi Mabaya Ya Ofisi

Meneja wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mkoa wa Dar es Salaam, Lawrence Mwalumwelo na wenzake wawili wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sophia Nyanda akishirikiana na Veronica Chimwanda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Ofisa Tawala, Modester Fumbuka na Ofisa Manunuzi, Radecunda Massawe, wafanyakazi wa TPC.

Chimwanda alidai kuwa kati ya Agosti Mosi na Oktoba 31, 2010 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuipa mkataba wa kutafuta vibarua kampuni ya Technical Merchantile Service bila kupata kibali kutoka bodi ya zabuni.

Vilevile ilidaiwa kuwa Septemba 26 ,2011 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuiongezea kampuni hiyo mkataba wa kutafuta vibarua kutoka Septemba 30 hadi Desemba 31, 2011 bila ya kuishirikisha bodi hiyo.

Ilidaiwa kuwa Januari Mosi, 2012 washtakiwa hao waliiongezea tena kampuni hiyo mkataba wa kutafuta vibarua kutoka Januari Mosi, 2012 hadi Machi 30, 2014 bila ya kuishirikisha bodi hiyo. Washtakiwa hao walikana mashtaka.

Washtakiwa hao waliachiwa baada ya kutumiza masharti ya dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Machi 17.
Rais Mugabe Atimiza miaka 92.....Wasaidizi wake Wasema Atawania Tena Urais Mwaka 2018

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametimiza umri wa miaka 92 huku chama chake kikisema atawania tena urais 2018.

Mnadhimu wake mkuu alisema kiongozi huyo ambaye ameongoza nchi tangu mwaka 1980, bado ana uwezo kamili wa kuongoza Serikali licha ya tetesi kwamba hawezi kuongoza kutokana na umri.

Akizungumza na gazeti la Serikali Sunday Mail, Katibu Mkuu wa Rais Misheck Sibanda alisema tetesi hizo si za kweli na hazina msingi kwani Mugabe ana ratiba ya wiki nzima kutekeleza kazi za Serikali na chama.

Rais Mugabe ambaye aliapa kuongoza nchi hadi atakapokufa, alishinda kipindi kingine cha urais cha miaka mitano kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 uliofanyika chini ya katiba mpya inayoweka ukomo wa kuongoza kwa vipindi viwili tu vya miaka mitano.

Chama chake tayari kimetangaza kumpitisha Mugabe kama mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Mugabe amekua kiongozi wa Zimbabwe tangu 1980. Ni mwenyekiti wa chama tawala cha Zanu. 1980 alikuwa waziri mkuu na 1987 Rais wa Zimbabwe.

Utawala wa Mugabe umeitwa wa kidikteta tangu mwaka 2002 kutokana na  kudharau haki za binadamu nchi Zimbabwe.
Samuel Sitta afuguka kuhusu Bandari

                                      Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania                                                                                  Samwel Sitta
Mwanasiasa mashuhuri na Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta, ameandika barua kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kueleza kuhusu mtazamo wake wa utumbuaji majipu katika Mamlaka ya Bandari za Tanzania (TPA), Raia Mwema limeambiwa.
Katika barua hiyo, Sitta ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Awamu ya Nne ameeleza kuwa ni vema serikali ikachunguza zaidi kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya TPA iliyovunjwa pamoja na menejimenti yake; kwa maelezo kwamba hawakuwa wakihusika na matatizo yaliyokuwepo kabla yao.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili wiki hii, Sitta amesema kwamba yeye anaunga mkono utendaji wa Rais John Magufuli na serikali yake; lakini anaamini kwamba kwa ujasiri uleule wa kutumbua majipu, serikali pia inapaswa kukubali kurejea maamuzi yake, pale inapobaini kuwa ilifanya makosa.
“ Katika barua yangu kwa Waziri Mkuu, kwa mfano, nimemueleza kwamba ile bodi ya TPA iliyovunjwa ilikuwa imefanya mkutano wake mara moja tu tangu iteuliwe. Kwa vyovyote vile, haiwezi kuwa inahusika na makosa yaliyotokea kabla yenyewe haijateuliwa.
“ Hivi sasa serikali ya Magufuli imebaini mianya kadhaa ya ukwepaji kodi kupitia bandari kavu yaani ICD lakini ukichunguza kwa makini, utaona kwamba ni menejimenti mpya ya TPA iliyoteuliwa ndiyo iliyofanya kazi ya kubaini mapungufu hayo. Sasa watu kama hawa, kwa maana ya bodi na menejimenti wanapoitwa majipu, inaumiza kwa kweli.
“ Kuna wanataaluma na watu ambao walikuwa wamejitolea, pamoja na vitisho na mazingira mengine magumu ya kazi, kuwa wazalendo na kutetea mali ya taifa. Hawa watu, kama wamekosea, sawa, lakini kama wamekaa kwenye bodi kwa kufanya kikao kimoja tu na baadaye kufukuzwa kwa namna ile, nadhani kuna haja ya kutazama haya mambo,” alisema Sitta ambaye sasa ametangaza kustaafu siasa.
Katika mazungumzo hayo, Sitta alisema anafahamu kuwa nia na dhamira ya serikali katika kupambana na ufisadi ni thabiti lakini yeye ametoa mawazo yake hayo kwa sababu ni mtu anayefahamu mazingira ya TPA na alihusika na uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo.
“Kuliko mtu mwingine yeyote, mimi nafahamu mazingira yaliyokuwepo pale TPA kabla ya bodi ile kuundwa. Mimi ndiye niliyevunja bodi iliyokuwepo na kuunda bodi mpya. Ninafahamu kuwa ilikutana mara moja tu, mwezi Oktoba na miezi miwili baadaye ndiyo imetangaza kuvunjwa.
“ Nyingi ya tuhuma zilizopo sasa kuhusu TPA na mambo mengine zilitokea kabla ya bodi ile kuundwa. Mimi ndiyo niliwaomba wale watu waje kusaidia kama wajumbe wa bodi. Sasa, kama mimi nisipojitokeza na kusema ninachokijua, huenda serikali isipate maelezo halisi. Ndiyo sababu nikaandika barua ile kwa Waziri Mkuu ambaye nafahamu amekuwa akifuatilia masuala ya bandari kwa karibu,” alisema.
Alisema utetezi wake kuhusu menejimenti unafanana na ule wa bodi kwa sababu ni menejimenti hiyo ndiyo iliyochunguza na kubaini matatizo –yaliyokuja kuwa sehemu ya ripoti aliyokabidhiwa Majaliwa kuhusu TPA na ambayo ndiyo inafanyiwa kazi na serikali hivi sasa.
Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa kuvunja bodi ya TPA, menejimenti pamoja na kutengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka. Uamuzi huo ulitangazwa na Majaliwa baada ya kufanya ziara bandarini mwezi Desemba mwaka jana.
Waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo ni Dk. Tulia Akson – Mhadhiri Mwandamizi, ambaye sasa ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Injinia Mussa Ally Nyamsigwa, Donata S Mugassa,
Haruna Masebu, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa EWURA, Injinia Gema Modu, Dk. Francis Michael ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Crescentius Magori ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango (NSSF) na Flavian Kinunda Mkurugenziwa Masoko Mstaafu, Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Profesa Joseph Msambichaka, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwezi Januari, mwaka 2013, akichukua nafasi ya Raphael Mollel, ambaye uteuzi wake ulikuwa umetenguliwa.
Menejimenti ambayo uteuzi wake umetenguliwa na Magufuli ilianza kazi Januari mwaka jana, kwa Awadh Massawe kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, akichukua nafasi ya Madeni Kipande.
Akizungumzia siku 100 za Magufuli, Sitta alisema amebaini ni kiongozi anayekwenda kwa kasi na viwango ambavyo yeye alitamani rais wa Awamu ya Tano awe navyo, na akatoa wito kwa Watanzania kumuombea kiongozi huyo ili atomize ndoto zake za kuondoa kero za wananchi.
Sitta alisema anafahamu kuwa kuna vikwazo na vitisho mbalimbali ambavyo Magufuli atapitia katika kutekeleza majukumu yake na akamtaka asiwe muoga na awe jasiri kwani Watanzania wote wako nyuma yake.
“Ombi langu kubwa kwa wasaidizi wake ni kuwa nao wanatakiwa waende na kasi yake. Nashukuru kuwa nimeona mawaziri wake wakitembelea sehemu na maeneo ambako kuna kero za wananchi. Huu ni mwanzo mzuri kwani wakimuacha peke yake, inaweza kuonekana kuwa wanapea,” alisema Sitta
CUF Yatangaza Maandamano Makubwa Dar es Salaam

Wanawake wa chama cha wananchi CUF maarufu kama JUKECUF wametangaza kufanya maandamano ya Amani siku ya tarehe 22,mwezi huu wa pili Jijini Dar es salaam yenye adhma ya kupinga hali ya kisiasa inayoendelea visiwani Zanzibar.

Akizungumza na wanahabari mapema leo mwenyekiti wa jumuiya hiyo  Mh severena mwijage amewaambia wanahabari kuwa maandamano hayo yataanzia ofisi kuu za CUF buguruni kuelekea ofisi ya makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu

Amesema kuwa jumuiya hiyo inatambua kwamba hali ya Amani iliyopo Zanzibar ikivurugika kwa kiasi kikubwa watakaoathirika ni kina mama na watoto hivyo wameona  ni bora kufikisha kilo chao hicho kwa makamu wa Rais ambaye ni Mwanamke mwenzao awasaidie.

Maandamano hayo yatapita barabara ya uhuru,ofisi ya mkuu wa mkoa Dar es salaam,karume,kariakoo,mnazi mmoja,Central polisi,barabara ya sokoine ,Bandarini,mahakama kuu,mahakama ya ardhi,Hadi ofisi ya makamu wa Rais.

Maandamano hayo bado hayajaruhusiwa na polisi licha ya polisi kupata barua kutoka CUF.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli Atembelea Shule ya Msingi Mbuyuni na Kuwaaga Rasmi Walimu Wenzie na Wanafunzi Aliokuwa Akiwafundisha
LEO Feb 17 2016, Mke wa Rais John Pombe Magufuli  Janeth Magufuli amewasili katika shule ya msingi Mbuyuni, Dar  kwa  ajili  ya  kuagana  na  walimu wenzake  pamoja  na  wanafunzi  aliokuwa  akiwafundisha


Shule  ya  Msingi Mbuyuni ni  shule ambayo Mama Magufuli alisoma kuanzia darasa la kwanza na baadaye mwaka 1995 kurudi tena kufundisha hapohapo  kwa miaka 17 hadi mumewe Rais Magufuli  alipochaguliwa  kuwa  Rais  wa  Tanzania.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akipokea zawadi ya saa toka kwa mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Mbuyuni, Mwalimu Dorothy Mwalecela , Oysterbay, jijini Dar es salaam wakati wa sherehe fupi ya kuwaaga rasmi walimu wenzake na wanafunzi wa shule hiyo
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akisikiliza risala toka kwa mwanafunzi wa shule ya Msingi ya Mbuyuni Oysterbay, jijini Dar es salaam wakati wa sherehe fupi ya kuwaaga rasmi walimu wenzake na wanafunzi wa shule hiyo

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akipokea zawadi toka kwa Afisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni katika Shule ya msingi ya Mbuyuni Oysterbay, jijini Dar es salaam wakati wa sherehe fupi ya kuwaaga rasmi walimu wenzake na wanafunzi wa shule hiyo
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akisikiliza maelezo ya utangulizi ya mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Mbuyuni, Mwalimu Dorothy Mwalecela , Oysterbay, jijini Dar es salaam wakati wa sherehe fupi ya kuwaaga rasmi walimu wenzake na wanafunzi wa shule hiyo
Bomba Kubwa La Kusambazia Maji Kutoka Chanzo Cha Maji Cha Ruvu Chini Lafika Jijini Dar Es Salaam
Juu na Chini - Mafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.

Huduma ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la Dar es salaam inatarajiwa kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu kufuatia kukamilika kwa kilometa 54.8 za mradi wa Ujenzi wa Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini.

Mradi huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania una jumla ya urefu wa kilometa 55.9.

Akizungumzia mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa bomba hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam na huku ikiwa imebakiza kilometa 1.1.

 Amesema ujenzi wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa siku kutoka lita milioni 182 ambazo zote zitasukumwa kuja jijini Dar es salaam.

 Aidha, amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za ufinyu wa eneo linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi vizuri katika eneo la mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha ,changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai mbalimbali ya wananchi katika maeneo hayo.

“Ni kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi kukawia kumalizika zikiwemo za wananchi kufungua kesi 17  Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA tumeshinda kesi 14  ndiyo maana tumepata haki ya kutumia njia hii kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.

Ameongeza kuwa lengo la mradi huu nikuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.

Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, Kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga bomba hilo nchini Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa yeye kama Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili kukamilisha kwa wakati.

Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika eneo la mradi hasa eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam kampuni ya JBG Gauff Ingenieure inafanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

“Tumejipanga kufanya kazi hadi usiku kupunguza muda,kazi iliyobaki ni ndogo, tunawahakikishia DAWASA tutaimaliza kazi hii mwishoni mwa mwezi huu” Amesisitiza.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi  wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini  kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambao umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam 

Nape amsimamisha kazi Mkurugenzi wa Habari na Meneja wa Vipindi TBC
                                   Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye  amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Matukio wa TBC Mbwilo Kitujime na Meneja wa Vipindi wa shirika hilo Bi. Edna Rajab na kuagiza kufumuliwa kwa idara nzima ya habari na matukio ya TBC kutokana na utendaji usioridhisha.

                                                                                                                                                                 HABARI KITAIFA...!!!
Ikiwa ni siku moja baada ya Alhad Mussa Salum ambaye ni Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kuunga mkono Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) kutangaza tarehe ya uchaguzi visiwani humo, Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania imepinga.

Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema, kuruhusu kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo ni kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi.
Sheikh Ponda amesema kuwa uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana haukuwa na mashaka kwa kuwa, waangalizi wa nje pia walithibitisha hilo.
“Ripoti za waangalizi wa ndani na nje zilithibitisha kuwa uchaguzi haukuwa na dosari. Kuna sababu gani ya kurudia uchaguzi,” amehoji Sheikh Ponda.
Wakati Sheikh Ponda akihoji sababu za ZEC kutaka kurudiwa kwa uchaguzi huo, Sheikh Alhad aliipongeza tume hiyo na kuongeza“tunaiomba ZEC kusimamia kazi hii kwa haki, uadilifu na umakini mkubwa…”
Sheikh Alhad jana alisema kuwa Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) linaunga mkono uamuzi wa ZEC kurudia uamuzi huku akikitaka Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimesusia uchaguzi huo, kushiriki.
CUF kwenye mkutano wake wa Baraza Kuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Januari mwaka huu kilieleza kususia uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu na kudai kuwa, hakuna sababu yoyote kwa chama hicho kushiriki. ZEC ilifuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo, Sheikh Ponda amesema kuwa, ZEC haikuwa na sababu ya kufuta uchaguzi kwa kuwa, baada ya tume hiyo kutangaza matokeo, haina mamlaka ya kufuta.
Pamoja na kupinga kurudiwa kwa uchaguzi, Sheikh Ponda Sheikh Alhad amepata wapi kauli ya Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed kuwa anaunga mkutano marudio ya uchaguzi Zanzibar.
Sheikh Alhad kwenye mkutano wake jana alisema “Hata kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Ahmad pia anaunga mkono suala la kufanyika uchaguzi wa marudio kwa mujibu wa barua yake aliyonitumia mimi .”
Sheikh Ponda ameeleza kwamba, Sheikh Farid hawezi kutoa kauli hiyo na kwamba kama Sheikh Alhad anayo barua hiyo, aitoe hadharani.
“Sio jambo rahisi kuamini kwamba Sheikh Farid anaweza kutoa kauli hiyo, sio jambo rahisi kabisa na kama ni kweli basi atoe ushahidi wake,”ameeleza Sheikh Ponda.
Pia Sheikh Ponda ameonesha kushangazwa na ZEC kuhalalisha matokeo ya Rais wa Muungano wa Tanzania sambamba na Wabunge wa Bunge la Muungano.
Shekh Ponda amesema kuwa uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake bado ni halali “Sisi kama Tasisi ya Waislamu tunapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.”
Amesema kuwa, taasisi hiyo imeunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa na CUF pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunusuru hali ya kisiasa visiwani humo na kutaka majadiliano yaendelee.
Shekh Ponda amemshauri Rais John Magufuli kutimiza ahadi yake aliyoitoa bungeni ya kushughulikia mzozo huo kwa kushirikiana na Maalim Seif Shariff Hamad na Dk. Ali Mohammed Shein.
Amesema kuwa, Rais Magufuli hajatoa tamko lolote na kwamba hajaeleza amefikia wapi katika kutatua mzozo huu.
Sheikh Ponda amesema kuwa kuna viashiria vya kuvunjika kwa amani visiwani humo kutokana na watu kuporwa haki zao na kwamba watakapoamua kuitafuata kutazuka vurugu.
Jaji Mkuu wa Kenya Dk Willy Mutunga ameshauri kuendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha Muungano wa Tanzania, huku akionesha hofu kuwa ukivunjika unaweza kuwa na athari kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Jaji Mutunga alitoa ushauri huo jana wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam.
“Tanzania ina kila cha kujivunia kwani hakuna ukabila, wanajivunia lugha yao, utamaduni na msimamo wa ujamaa. Sidhani kama mmeingia katika ubepari na ukabaila,’’ alisema Jaji huyo na kuongeza kuwa msimamo wa Mwalimu Julius Nyerere ulijali maslahi ya wengine katika masuala mbalimbali ikiwemo uchumi na siasa.
Aidha, alisema Tanzania inafanya vizuri kuliko Kenya katika masuala ya usikilizaji wa kesi. Alisema watajifunza namna ya kusikiliza kesi haraka ili kumaliza mashauri kwa muda.
“Kenya iliwahi kusikiliza kesi tatu kwa zaidi ya miaka 33 hivyo ni tofauti na wanavyofanya wenzetu Watanzania,’’ alisema Jaji Mutunga na kusisitiza kuwa katika Afrika Mashariki, majaji na mahakimu wengi hawachukui rushwa na kwamba njia nzuri ni kuwatoa wanaopokea rushwa.

Wabunge wageuza Bunge uwanja wa mipasho


                                                       Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania mjini Dodoma

Ukumbi wa Bunge juzi uligeuka uwanja wa malumbano na mipasho huku misemo ikichukua nafasi kubwa kutoka kwa wabunge wa chama tawala CCM na upinzani.
Malumbano hayo yalizuka baada ya Bunge kukaa na kujadili Mwelekeo wa Mpango wa Taifa, lakini ghafla wabunge walianza kurushiana maneno wakituhumiana kuwa majipu yanayotakiwa kutumbuliwa.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti, Mary Mwanjelwa, malumbano yalianza kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe jambo lililoamsha mjadala mzito.
Kishoa alianza kumtaja Dk Mwakyembe kuwa ni jipu linalohitaji kutumbuliwa na Rais na kuwa nafasi aliyonayo hakustahili.
Kishoa alitaja sababu ya kumwita Dk Mwakyembe si msafi kwamba alitumia zaidi ya Sh238 bilioni kwa ajili ya kununulia mabehewa ambayo yalithibitika kuwa ni mabovu.
Kitendo hicho kiliamsha hasira za Dk Mwakyembe na kusimama kisha kukana Serikali kutumia kiasi hicho huku akisisitiza ikithibitika kuwa ni kweli yuko tayari kujiuzulu wadhifa huo.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Jenista Mhagama alisimama mara kadhaa kutaka Kishoa afute kauli lakini upinzani ulimtetea mbunge huyo.
Hata hivyo, Mwanjelwa aliwataka kuendelea na mjadala ili akaangalie kwanza kumbukumbu za Bunge kuhusu maneno yaliyotamkwa na baadhi ya wabunge.
ICC kumhukumu aliyekuwa Makamu wa Rais DRC


Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imesema itatoa hukumu dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Pierre Bemba anayekabiliwa na tuhuma za jinai za kivita, tarehe 21 mwezi ujao wa Machi.
Hukumu dhidi ya Bemba ni ya kwanza dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani katika mahakama hiyo ya kimataifa iliyobuniwa mwaka 2002 mjini Hague nchini Uholanzi, ili kukabiliana na makosa ya jinai na haswa ya kivita.
Bemba anakabiliwa na mashtaka matatu ya jinai za kivita na mawili dhidi ya binadamu, anayodaiwa kufanya kati ya Oktoba 2002 na Maci 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Makamu wa rais wa zamani wa DRC anakabiliwa na mashtaka ya kutenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu kwa kuwatuma wapiganaji wa MLC katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2003 ili kusaidia kuzima mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa wakati huo, Ange -Felix Patasse.
Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Afrika AU umepasisha pendekezo la serikali ya Kenya la kutaka nchi wanachama wake zijiondoe kwenye Mkataba wa Roma, uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

No comments :