Monday, February 15, 2016

Vyama nane vyajitoa rasmi Uchaguzi Zanzibar

                                                                                  Mwenyekiti wa ZEC Jecha Salum Jecha
Vyama nane ambavyo vimeungana na Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar, vimeiandikia rasmi Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kuwa havitashiriki uchaguzi huo. Vyama vilivyochukua uamuzi huo ni Chauma, DP, Demokrasia Makini, SAU, Jahazi Asilia, NRA, UPDP na UMD.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chauma, Mohamed Massod Rashid, alisema uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, una viashiria kuwa ushindi utakuwa ni wa kulazimisha na kwamba marudio hayo ni batili kisheria.
“Vyama vyetu vinajiondoa rasmi kwa kuthibitisha wagombea wetu hawatashiriki katika ngazi zote za uchaguzi wa marudio, pia hatutohusika kuwamo kwenye karatasi za kura pamoja na kupokea machapisho yoyote na matokeo ya uchaguzi,” alisema.
“Taarifa ya kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu iliyochapishwa katika gazeti la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Novemba 6, mwaka jana chini ya kifungu cha 119 (10) cha Katiba na vifungu 3(1) na 5 (a) vya sheria havikufuatwa na vilikiukwa na kuvunjwa na Mwenyekiti wa Tume,” alisema.
Alisema kuharibu uchaguzi ni kosa la jinai na inapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwafikisha mahakamani wahusika ili sheria ichukue mkondo wake, lakini inashangaza kuona watu waliohusika bado wanapewa nafasi ya kuandaa uchaguzi wa marudio.
“Ni wajibu wa tume ya uchaguzi kuzingatia matakwa ya sheria zinazosimamia uchaguzi, na haiwezekani kuepuka misingi na matakwa ya wananchi katika kuchagua viongozi wanaowataka, tume haina mamlaka na uwezo wa kutengua au kufuta uchaguzi na matokeo ambayo yameshakamilika na kutangazwa, chombo chenye mamlaka ya kutengua na kufuta matokeo ni Mahakama Kuu Zanzibar,” aliongeza kusema.
Naye, Mwenyekiti wa Jahazi Asilia na mgombea urais Zanzibar, Kassim Bakar Ali, alisema Rais Dk. John Magufuli hana namna ya kukwepa suala la Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama anajitenga nalo, anapaswa kuondoa majeshi na polisi visiwani humo.
Aidha, alisema pia hawatashiriki uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Kijitoupele unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi (Nec) hadi watakapopewa vitambulisho vya kupigia kura vinavyotolewa na tume hiyo na siyo vilivyotolewa na ZEC.
Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, kwa kueleza kuwa uligubikwa na kasoro mbalimbali ikiwamo wapigakura kuzidi.

No comments :